
Burundi yapiga kura ya maoni kubadilisha katiba
Raia wa Burundi leo wanapiga kura ya maoni ya kubadilisha katiba, hatua ambayo itaweza kumpa Rais Piere Nkurunziza nafasi ya kuwa rais hadi mwaka 2034.
Wananchi wa Burundi wamejitokeza leo kushiriki mchakato wa kupiga kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba. Mabadiliko hayo ya katiba, yatakampa nafasi Rais Pierre Nkurunziza kuweza kutawala hadi 2034. Mchakato huo unafuatiliwa kwa karibu hasa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu. Hatua hiyo imezua hofu ya ukandamizaji mkubwa wa kisiasa na migogoro ya kikabila katika taifa hilo la Maziwa Makuu.
Karibu watu nusu milioni wamekimbia tokea Nkurunziza kushinda muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi uliokuwa na ghasia wa mwaka 2015.
Nkurunziza, mwalimu wa zamani wa riadha na aliyekuwa kiongozi wa vita vya msituni kutoka katika kabila la wengi la Hutu, amekuwa akiliongoza taifa hilo tokea mwaka 2005 vilipomalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 300,000.