
Mhe. Zitto aikaba koo serikali ya Magufuli, atoa ushauri…
Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe amepingana na maamuzi ya serikali ya kukataa kuongeza mishahara ya wafanyakazi kwa kudai kuwa kuongeza mshahara kila mwaka kwa wafanyakazi ni suala la kisheria na ni la lazima.

Zitto Kabwe
Mhe. Zitto ametoa maoni hayo leo Mei 01, 2018 kupitia ukurasa ukurasa wake wa mtandao wa Twitter ambapo amesema serikali ni lazima iongeze mishahara ili wafanyakazi waweze kumudu gharama za maisha ikiwemo mfumuko wa bei.
“Kupandisha mishahara ya Wafanyakazi ni suala la kisheria. Kiutaratibu Serikali inapaswa kupandisha mishahara kila mwaka kulingana na mfumuko ya Bei ili kulinda nguvu ya manunuzi ya Mfanyakazi. Vyama vya Wafanyakazi HAVIPASWI kukubali maelezo ya kisiasa.“ameandika Zitto.
Hata hivyo, Zitto amevishauri vyama vya Wafanyakazi nchini kupingana na maamuzi hayo ya serikali “Vyama vya Wafanyakazi havipaswi kukubali maelezo ya kisiasa”.
Kauli ya Mhe. Zitto Kabwe imekuja yakiwa ni masaa machache yamepita baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza kuwa serikali haitaongeza mishahara ya wafanyakazi kwa mwaka huu.