Ofisa Ardhi wilaya ya NAMTUMBO apewa mwezi mmoja kufidia…
WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya NAMTUMBO Bwana MAURUS YERA awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha LWINGA wilayani humo.
Wakazi hao 21, mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilichukuliwa na Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ya mkoa wa RUVUMA na waliahidiwa kulipwa fidia.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa LWINGA akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani RUVUMA.
Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango, ambapo wamemuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.
Waziri Mkuu amesema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Daktari John Magufuli inataka kila mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.