
TABORA: Agizo la Rais Daktari JOHN POMBE MAGUFULI kuhusu…
Bodi ya Filamu katika halmashauri ya manispaa ya TABORA imepanga kukutana kuweka mikakati ya kusimamia maadili ya uvaaji kwa wasanii wa kizazi kipya baada ya Rais Daktari JOHN POMBE MAGUFULI kuagiza taasisi zinazohusika kusimamia uvaaji kwa wasanii wa kike.
Katibu wa Bodi ya Filamu wa wilaya ambaye ni Afisa Utamaduni wa manispaa ya TABORA,MEDERICKO KATUNZI amesema atazungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu ili kupanga namna watakavyosimamia maadili ya mavazi ya wasanii wa kike.
KATUNZI ameongeza kuwa manispaa ya TABORA imekuwa na wasanii chipukizi ambao wanaiga mavazi ambayo yanaacha wazi viungo vyao vya mwili jambo ambalo ni la aibu katika jamii.
Nao baadhi ya wasanii mjini TABORA, KULWA, KASELE RAMADHANI,ANASTAZIA LINUS na RASHIDI MAGEDULA wamesema agizo la Rais MAGUFULI kwa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi mapema wiki hii kuhusu uvaaji wa nusu uchi kwa wasanii wa kike lipo sahihi kutokana na wasanii kukubuhu na uvaajihuo usiofaa.
Naye mmoja wa wakazi wa Manispaa ya T ABORA,FABIANO ALFRED amesema wasanii hawana budi kubadilika katika uvaaji wao kwa sababu wao ni kioo cha jamii na pale wanapokwenda kinyume na maadili wanapotosha umma.
Akufungua mkutano mkuu wa tisa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi,Jumanne wiki hii mjini DODOMA Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais MAGUFULI alieleza kukerwa kwake na Mamlaka zinazohusika na maadili kutochukua hatua dhidi ya wasanii wanaoimba majukwani wakiwa na mavazi ya nusu uchi na kumtaka Mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo kuhakikisha anasimamamia maadili ya vijana na Taifa kwa jumla.