
TABORA: Wanawake waipongozea CGFM kwa Mchezo wa KIBUBU CHALENGE
Wanawake wa mkoa wa TABORA wameipongeza CGFM kwa kuanzisha mchezo wa Radio wa KIBUBU CHALLENGE ambao unawanufaisha katika jitihada za kujiletea maendeleo.
Wakizungumza katika Studio za CGFM wakati wakikabidhiwa VIBUBU kwa ajili ya kujiwekea akiba, wanawake RABIA ROMANA,FABIOLA MSELE na ANITHA JULIUS wamesema hiyo ni hatua mojawapo ya CGFM kuwathamini wanawake ambao ni wajasiriamali wadogo ili wafahamu njia bora ya kujiwekea akiba na hatimaye wakuze biashara zao.
Mratibu Mkuu wa Mchezo huo wa KIBUBU CHALLENGE,NAJJAT OMARI amesema mchezo huo ni moja ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Machi Nane ikilenga kuwahamasisha wanawake kujishughulisha na kuacha kuwa utegemezi katika jamii zao.
Amewataka wanawake ambao wanajishughulisha na biashara ndogondogo waje kuchukua VIBUBU kwa uaminifu kwa sababu watafuatiliwa ili kujiridhisha kama wana kipato cha chini ili kuepuka udanganyifu katika mchezo huu.
Mchezo wa Radio unaojulikana kama KIBUBU CHALLENGE na Siku ya Wanawake Duniani inayoratibiwa na CGFM kupitia hafla ya CG WOMEN GALA vinalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi hasa wajasiriamali wadogo wenye mtaji usiozidi shilingi elfu hamsini na faida isiyozidi shilingi elfu kumi kwa siku.