
Trump adokeza kukutana na Kim katika jumba la amani
Rais wa Marekani Donald Trump amedokeza kuwa mkutano wa kilele unaotarajiwa kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ufanyike katika nyumba ya amani iliyoko katika mpaka kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini, eneo ambalo Kim alikutana na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in wiki iliyopita.
Kupitia ukurasa wa Twitter, Trump amesema maeneo mengi katika nchi chungu nzima yanadhaniwa kuwa maeneo muafaka ya mkutano lakini anadhani nyumba ya amani itakuwa yenye ishara muhimu zaidi kuliko mkutano huo kufanyika katika nchi nyingine.
Trump anatarajiwa kukutana na Kim katika wiki chache zijazo. Hayo yanakuja huku Rais wa Korea Kusini Moon Jae in akisema Trump anastahiki kupewa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na juhudi zake za kuutatua mzozo juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.