Walemavu wa Ngozi mkoani TABORA watakiwa kushiriki katika huduma…
Watu wenye ulemavu wa ngozi-ualbino mkoani TABORA wametakiwa kushiriki katika huduma za kliniki kwa ajili ya kupewa elimu sahihi ya matumizi ya mafuta ya kujikinga na mionzi ya jua na jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa saratani ya ngozi.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa huduma za afya kutoka shirika la STANDING VOICE,KABALA MAGANJA akisema watu wanaoishi karibu na kliniki za matibabu ya watu wenye ualbino watumie fursa hizo kenda vituoni ili watibiwe.
Katika hatua nyingine ameitaka jamii kutambua umuhimu wa watu wenye ualbino kwa kuwa mstari wa mbele kupinga mauaji na hata kuwapatia elimu watoto wenye ualbino.
Kwa upande wake,Katibu wa chama cha watu wenye ualbino mkoa wa TABORA RAMADHANI MLAMBA amewasihi watu wenye ualbino kujitokeza kwa wingi katika kliniki hizo na matibabu ili waweze kujua njia sahihi za kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Shirika la STANDING VOICE linatoa huduma kwa watu wenye ualbino katika vituo vitano Mkoani TABORA ambavyo ni Hospitali ya rufaa ya mkoa wa TABORA-KITETE,shule ya msingi FURAHA, shule ya sekondari TABORA WASICHANA,Hospitali ya wilaya ya NZEGA na Hospitali ya wilaya ya URAMBO.
Katika zoezi hilo la utoaji wa huduma kwa watu wenye ualbino ambalo limeanza kutolewa katika vituo hivyo linaambatana na utoaji wa elimu,vifaa kama kofia,miwani na mafuta ya kupaka ili ya kujikinga na mionzi ya jua kwa lengo la kuzuia saratani ya ngozi kwa watu hao.