
Watu wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti Mkoani TABORA
Kamanda wa polisi mkoa wa TABORA kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi WILBROAD MUTAFUNGWA amesema tukio la kwanza limetokea katika wilaya ya IGUNGA ambapo MIPAWA LUFUNGA ameuawa kwakuchomwa kisu.
Amesema kufuatia tukio hilo wananchi kwa kushirikiana na jeshi la polisi wamemtia mbaroni mtuhumiwa huyo na anaendelea kuhojiwa katika kituo cha polisi IGUNGA na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Katika tukio jingine Kamanda MUTAFUNGWA amesema mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MICHAEL PETER mkazi wa kata ya CHEMCHEM amegundulika amekufa kwenye kilabu cha pombe za kienyeji mtaa wa MASEMPELE kata ya NGAMBO Manispaa ya TABORA.
Awali akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa wa MASEMPELE kata ya NG’ AMBO SHABAN KAOMBWE amekiri kuwa alipata taarifa za tukio hilo mapema na alitoa taarifa kwa jeshi la polisi kwa msaada zaidi.
Kwa upande wake mjumbe wa serikali ya mtaa wa MASEMPELE NASORO JUMA amesema mtaa huo unaongoza kwa matukio ya mauaji hivyo ameiomba serikali iwasaidie kutokana na mtaa huo kuwa na vijana wengi wanaocheza kamali.
Kwa mujibu kamanda wa polisi mkoa wa TABORA wana mkakati wa kuangalia mambo yanayochangia matukio ya kihalifu hasa ya utengenezaji na utumiaji wa pombe za kienyeji ikiwemo gongo
Na wanaendelea na misako ili kuhakikisha wananchi wanakunywa pombe zilizopimwa na kukaguliwa na shirika la viwango nchini TBS.