Baadhi ya shule Mkoani TABORA zimeweka mazingira mazuri kwa…

Baadhi ya shule Mkoani TABORA zimeweka mazingira mazuri kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujisitiri wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Mkoa wa TABORA Bi SUZAN NUSU akisema kuwa mikakati inaendelea kuhakikisha kila shule inakuwa na chumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi ambao wamefikia umri wa kubalehe.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari KAZIMA Mwalimu MRISHO KIVURUGA amesema katika shule hiyo wanafunzi hutumia chumba cha Matroni kama chumba cha huduma ya kwanza wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Kwa upande wake mwanafunzi wa darasa la sita ambaye amepewa jina la SIKUJUA KAMBA siyo jina lake halisi wa shule ya msingi CHEMCHEM Manispaa ya TABORA anaeleza adha anayopata anapokuwa katika hedhi akiwa mazingira ya shuleni.
Mwalimu wa mazingira MAHALALA NICHOLAUS na mwalimu wa afya AGNESS LUGONDA wa shule ya sekondari KAZEHILI wameziomba asasi mbalimbali kuwasaidia kutoa vifaa kama pedi na dawa ambazo zitawasaidia wanafunzi watakapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Kwa mujibu wa mwalimu wa taaluma shule ya msingi CHEMCHEM HELENA YESSE wanafunzi wa kike hukosa masomo kutokana na tatizo la hedhi ambapo shule zimetakiwa kuweka mazingira wezeshi ili kuwasaidia wanafunzi wa kike kujistiri wakiwa kwenye hedhi.