
Diwani wa kata ya KABILA ajiuzulu na kujiunga na…
Mwandishi: Hassan Kitunga.
Aliyekuwa diwani wa kata ya KABILA katika Halmashauri ya Manispaa ya TABORA kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA, ADAM KALONGA amejiuzulu uongozi na kujiunga na Chama cha Mapinduzi –CCM baada ya kuridhishwa na uongozi wa Rais Daktari JOHN POMBE MAGUFULI.
Akizungumzia uamuzi wake wa kujiuzulu udiwani wa CHADEMA mbele ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya TABORA,KALONGA amesema Chama cha Mapinduzi kinatekeleza matakwa ya wananchi na ni chama pekee chenye kuleta maendeleo,hivyo ameamua kurudi ili kumuunga mkono Rais Daktari JOHN MAGUFULI.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya TABORA,MOHAMED KATETE amemkaribisha Diwani KALONGA na kwamba sasa yupo katika chama imara chenye kuleta maendeleo kwa wananchi.
Naye Katibu wa Uenezi,Itikadi na Siasa wa CCM wilaya ya TABORA,RASHID RAMADHAN maarufu kama Kamanda TALL amesema Chama cha Mapinduzi kina sera nzuri na kinatakeleza ilani ya chama hicho.
Akizungumzia hatua ya diwani huyo kukihama chama cha CHADEMA,Katibu wa CHADEMA wilaya ya TABORA,MSABAHA KAMBAMBOVU amesema chama hicho kilimvua uanachama tangu Januari 27 mwaka huu.
Kauli ya Katibu huyo wa CHADEMA yamepingwa vikali na Diwani KALONGA akisema hajavuliwa uanachama bali ameamua mwenyewe kujiunga na CCM.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa CCM wilaya ya TABORA,ADAM KALONGA aliwahi kuwa mwanachama wa CCM na baadaye akajiunga na CHADEMA na baada ya kuona amepotea njia ameamua kurudi tena katika Chama cha Mapinduzi.