
Jeshi la polisi mkoani TABORA likishirikiana na Wamiliki wa…
Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoni TABORA limesema mpango ulionzishwa na jeshi hilo kwa kushirikiana na wamiliki wa vituo vya mafuta wa kutowapatia huduma ya mafuta waendesha pikipiki wasiokuwa na kofia ngumu utafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kamanda wa polisi kitengo cha usalama barabarani,Mrakibu wa polisi EMILIAN KAMUHANDA amesema wanatambua changamoto zilizopo kwa waendesha pikipiki na kwamba jeshi la polisi litafuatilia katika vituo vyote vya mafuta na kuwachukulia hatua waendesha pikipiki watakaokiuka utaratibu uliowekwa.
Amesema lengo la mpango huo ni kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikipoteza nguvu kazi ya taifa na kwamba waendesha pikipiki wanapaswa kutekeleza mpango huo.
Naye mwenyekiti wa waendesha pikipiki katika kata ya KIDONGO CHEKUNDU SAIDI HAMISI amelipongeza jeshi la polisi kwa kuanzisha mpango huo na kuwasihi waendesha pikipiki wenzake kuzingatia sheria.
Nao baadhi ya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda mbali na kupongeza mpango huo,wameliomba jeshi la polisi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo kwa sababu kuna baadhi yao hawatekelezi.
Kwa upande wao baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta mjini TABORA wamesema kuna baadhi ya bodaboda hawatekelezi agizo hilo na kwamba kutokana na maagizo ya jeshi la polisi wanagoma kuwauzia mafuta bila ya kuwa na kofia ngumu.
Tarehe mosi mwezi huu jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoani TABORA kwa kushirikiana na wamiliki wa vituo vya mafuta walianzisha operesheni ya mwendesha pikipiki asiye na kofia ngumu maarufu kama Helment kutopewa huduma ya mafuta.