
Macron na Putin wajadili makubaliano ya nyuklia ya Iran
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakutana na Rais Vladimir Putin kujaribu kuyanusuru makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran baada ya Marekani kujiondoa kutoka makubaliano hayo ya kimataifa.

Macron atafanya mazungumzo na Putin kuhusu suala hilo la Iran licha ya kuwepo tofauti kubwa kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Urusi kuhusu masuala mbali mbali ya kimataifa kuanzia mzozo wa Syria, wa Ukraine na madai ya Urusi kuingilia chaguzi.
Nchi za Ulaya kuyanusuru makubaliano ya Iran?
Lakini viongozi hao wawili wote wanasemekana kuwa na ari ya kuyanusuru makubaliano kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo, Urusi, China, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Marekani kudhibiti shughuli za kinyuklia za Iran na badala yake nchi hiyo ilegezewe vikwazo vya kiuchumi.
Macron na Putin watajadiliana pia uhusiano wa kiuchumi licha ya vikwazo dhidi ya urusi vilivyowekwa baada ya kuinyakua rasi ya Crimea.
Na suala hilo la Iran ndiyo mara ya kwanza Urusi, Ufaransa na Ujerumani zinakuwa na msimamo mmoja kuhusu suala lenye uzito wa namna hiyo katika safu ya kimataifa katika kipindi cha miaka kadhaa sasa.
Aidha leo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa China Li Keqiang wameyatetea makubaliano hayo ya kinyuklia. Li amesema kusambaratika kwa makubaliano hayo ya Iran kutahujumu pia juhudi za kuitaka Korea Kaskazini kukomesha mpango wake wa kinyuklia.
Iran yatoa masharti
Kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei leo amewahutubia maafisa wa serikali na kutoa muongozo wa masharti ambayo nchi hiyo inataka nchi zenye nguvu zaidi duniani zilizosalia katika makubaliano hayo kuyazingatia iwapo zinataka kuyanusuru.
Ali Khamenei amesema kujiondoa kwa Marekani kutoka makubaliano hayo ni ukiukaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2231 lililopekea kufikiwa kwa makubaliano hayo na kuzitaka nchi za Ulaya kuwasilisha azimio katika baraza hilo kupinga hatua ya Marekani.
Pia amewataka viongozi wa nchi tatu za Ulaya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuahidi kutopinga ushawishi wa Iran katika kanda ya Mashariki ya Kati au kuwepo kwa mpango wake wa kinyuklia kwani kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa Iran inanuia kudumisha mpango huo kwa minajili ya kujilinda, akiahidi watarejelea shughuli zao za kutaka kuzalisha asilimia 20 ya madini ya Urani iwapo makubaliano hayo yatafeli.
Iran pia imetaka nchi za Ulaya kuahidi kuwa itanunua mafuta yake iwapo Marekani itafanikiwa kutatiza uuzaji wa mafuta kupitia kuiwekea tena vikwazo. Khamenei amesema Iran haitafuti mkwaruzano na nchi za Ulaya lakini kutokana na mienendo yake katika kipindi cha nyuma hawawezi kuwaamini na kutokana na hilo wanataka kupata hakikisho thabiti.
CHANZO: DW Idhaa ya Kiswahili.