
Makubaliano kuhusu nyuklia ya Iran yana kasoro.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema nchi za Umoja wa Ulaya zinakubali kwamba Makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yana mapungufu, lakini pia zimekubaliana kuwa yanapaswa kuendelezwa.
Viongozi wa nchi 28 za Umoja wa Ulaya wanaokutana katika mji mkuu wa Bulgaria Sofia, wameweka mshikamano katika kuyanusuru makubaliano hayo yaliyosainiwa mwaka 2015, baada ya Rais Donald Trump kuiondoa Marekani, na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, akilalamikia mpango wa makombora wa nchi hiyo na kujiingiza kwake katika mizozo ya Mashariki ya Kati.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia amesema Ulaya inafanya juhudi kuyaokoa makubaliano hayo, ili iweze kuendeleza biashara na Iran. Iran imetoa tahadhari kwamba inaweza kuanzisha urutubishaji wa madini ya Urani bila kikomo, ikiwa Ulaya itashindwa kuihakikishia kwamba faida zitokanazo na kuondolewa kwa vikwazo chini ya makubaliano hayo zitaendelea kupatikana.