
Marekani kuiwekea EU ushuru katika bidhaa
Marekani imesema itaweka ushuru katika bidhaa za chuma cha pua na bati zinazoingizwa kutoka nchi za Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico kuanzia usiku wa kuamkia kesho.
Waziri wa Biashara wa Marekani, Wilbur Ross amesema leo kuwa mazungumzo na Umoja wa Ulaya yameshindwa kufikia makubaliano ya kuridhisha kuishawishi Marekani kuendelea na msamaha wa ushuru wa forodha uliowekwa mwezi Machi.
Mexico nayo imetangaza kuweka viwango vipya vya ushuru dhidi ya Marekani wakati Umoja wa Ulaya ukisema hatua ya Marekani dhidi ya Umoja huo haikubaliki. Ross amesema mazungumzo na Canada na Mexico ya kuuangalia upya Mkataba wa Biashara Huria, NAFTA, yanachukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa na hakuna tarehe maalum iliyowekwa ya kukamilika kwa mazungumzo hayo, hivyo msamaha wao pia utaondolewa.
Amebainisha kuwa asilimia 25 ya ushuru itawekwa katika bidhaa za chuma zitakazoingizwa Marekani na asilimia 10 katika bidhaa za bati.