
Rais Daktari JOHN MAGUFULI amewasisitiza watanzania kuendelea kulipa kodi…
Rais Daktari JOHN POMBE MAGUFULI amewasisitiza watanzania kuendelea kulipa kodi ili kuwezesha miradi mbali mbali kutekelezwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa-Standard Gauge.
Akizungumza katika stesheni ya IHUMWA wakati wa uzinduzi na uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya pili kutoka MOROGORO hadi MAKUTUPORA mkoani DODOMA,Rais MAGUFULI amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuajiri Watanzania wengi.
Awali akitoa salamu za mkoa,mkuu wa mkoa wa DODOMA, BINILITH MAHENGE amesema wameanza kuwaandaa vijana ili wanufaike na ujenzi wa reli ya kisasa na kwamba wananchi wa DODOMA hawatamwangusha Rais MAGUFULI.
Kwa upande wake,Balozi wa UTURUKI,ALI GAITOL amesema ujenzi wa reli ya kisasa siyo tu utarahisisha usafirishaji,lakini pia utachochea maendeleo ya nchi na utasaidia kuimarisha mahusiano kati ya serikali ya UTURUKI na TANZANIA katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli TANZANIA-TRC-, MASANJA KADOGOSA amesema kutokana na kasi ya ujenzi wa reli hiyo,baadhi ya wananchi watafuatwa na kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa reli.
Mbunge wa DODOMA Mjini,ANTONY MAVUNDE ameipongeza serikali ya Awamu ya Tano akisema kuwa ni sikivu kwa sababu imesaidia jimbo lake kupata huduma ya maji huku akiahidiwa kupata umeme mkoa mzima.
Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi,Profesa MAKAME MBARAWA amesema hadi sasa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa umeajiri Watanzania 2,100 ambayo ni fursa kwa wananchi.
Ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa-STANDARD GAUGE ulianza rasmi Februari 26 mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Februari 25 mwaka 2021.