
Serikali imeshauriwa kutekeleza sheria kwa watu wanaofanya vitendo vya…
Serikali imeshauriwa kutekeleza sheria kwa watu wanaofanya vitendo vya ukatili ili kutokomeza tatizo hilo katika jamii. Wito huo umetolewa na ROSEMARY SILILI wakati wa zoezi la kalamu na ubao linaloendeshwa na CGFM katika kata ya MAPAMBANO,eneo la SOKONI ikiwa ni sehemu ya kampeini yake ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Amesema endapo elimu itatolewa kwa watu sambamba na utoaji wa adhabu kali kwa watu wanaofanya vitendo vya ukatili basi wengi wao wataogopa kujihusisha na vitendo hivyo.
Kwa upande wake RASHIDI MAKULA amewashauri vijana wa jinsia zote kuzingatia maadili hasa katika kuvaa mavazi ya heshima ili kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
Naye PRISCA RICHARD amemuunga mkono akisema wanawake wanaovaa mavazi yasiyo ya maadili yanawadhalilisha katika jamii inayowazunguka.
Hali kadhalika,JOHARI HASSAN amesema vitendo vingine vya ukatili wa kujinsia wanavyofanyiwa wanawake ni kutokana na wanaume kutelekeza familia zao kwa kigezo cha kuwa na maisha magumu.
Akizungumzia malalamiko ya wanaume kuwatelekeza wanawake, RASHIDI MAKULA amesema wanaume hufanya hivyo kutokana na manyanyaso wanayofanyiwa na wenza wao.
Wanawake na watoto mkoani TABORA ni makundi ambayo hufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa kama ubakwaji na kulawitiwa jambo ambalo limetakiwa kupingwa na wananchi kwa nguvu zote.