
Serikali kuendelea kuratibu mpango wa kutoa chaakula Shuleni.
Serikali imesema inaendelea kuratibu mpango utakaowawezesha kuanza kutoa chakula shuleni kwa wanafunzi wa shule za sekondari za kutwa na shule za msingi ili wanafunzi waweze kusoma vizuri.
Waziri Mkuu,KASSIM MAJALIWA ameeleza hayo bungeni jijini DODOMA wakati akijibu maswali ya papo kwa papo ambapo amesema suala la chakula ni muhimu kwa wanafunzi lakini serikali haiwezi kutoa chakula kwa shule zote zilizopo nchini.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa TEMEKE,ABDALA MTOLEA ambaye alitaka kujua ni lini serikali itabadilisha sera ya elimu bure ili chakula shuleni liwe suala la lazima.
Waziri Mkuu amesema mpango wa elimu bure unaratibiwa kadri ya mahitaji na kuwa suala la chakula kwa sasa wazazi wanaweza kuona umuhimu wa kupeleka chakula shuleni.
Waziri Mkuu amewasihi wazazi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau katika kuimarisha elimu na kutafuta njia bora ya kuboresha elimu ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa watoto ili waweze kusoma vizuri na kwamba siyo lazima chakula kiwe wali au ugali hata uji unatosha.