
TABORA: Halmashauri ya Manispaa ya TABORA imeshauriwa kuweka utaratibu…
Halmashauri ya Manispaa ya TABORA imeshauriwa kuweka utaratibu mzuri wa uzoaji wa taka katika dampo la KACHOMA ili kukabiliana na mrundikano wa uchafu unaokuwepo mara kwa mara.
Baadhi ya wafanyabiashara katika soko la KACHOMA,SAIDI JUMA na SHABANI MASHAKA wamesema mrundikano wa uchafu katika eneo hilo unatokana na kutozolewa taka kwa wakati na idadi ndogo ya makontena.
Naye mfanyabiashara mwingine katika soko hilo,HALFAN KABATA amesema dampo la KACHOMA linasababisha wadudu wasambae maeneo ya biashara zao.
Kwa upande wake,Katibu wa soko hilo,ALI KAFWIMBI amesema tatizo kubwa linalochangia mrundikano wa taka katika dampo hilo ni kuwepo kwa gari moja pekee la kuzolea taka.
Amewataka wananchi kuacha tabia ya kumwaga takataka katika eneo hilo na kwamba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake kwa sababu viongozi wana majukumu mengi hivyo ni vigumu kuwasimamia kutomwaga uchafu katika eneo hilo.