
TABORA: Mkuu wa Mkoa awapongeza wazazi, walezi na walimu…
Mkuu wa mkoa wa TABORA,AGGREY MWANRI amewapongeza walimu,wazazi na walezi kwa kushirikiana vema kupandisha ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba,kidato cha nne na sita.
Katika salamu zake kwa wananchi wa mkoa wa TABORA za kumaliza mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018,MWANRI pia amewataka wazazi na walimu kuendelea kushirikiana kufuatilia mwenendo wa wanafunzi ili kuendelea kupandisha ufaulu kwa mwaka huu.
Akizungumzia sekta ya Afya,mkuu wa mkoa wa TABORA amesema pamoja na mapungufu yaliyojitokeza mwaka uliopita ukiwemo uhaba wa dawa na baadhi ya vituo vya afya kutowahudumia wagonjwa vizuri, serikali imejipanga kuondoa kasoro hizo.
Amesema tatizo lingine ni watu kuugua matumbo na minyoo mkoani TABORA kutokana na kutonawa mikono kabla ya kula hivyo amewataka kuzingatia hilo ili kupunguza magonjwa yanayozuilika.
Kuhusu mazingira amewashukuru wananchi wa mkoa wa TABORA,kituo cha Radio cha CGFM na waandishi wote wa habari mkoa huu kwa kushiriki vema kufanikisha kampeni ya upandaji na utunzaji wa miti mwaka 2017.
Ameongeza kuwa mwaka 2018 ili uwe wa mafanikio na maendeleo zaidi katika sekta mbalimbali,kila mmoja hana budi kusimama katika nafasi yake na kwa ushirikiano na jamii.