
TABORA: Watumishi wa serikali kutakiwa kuwa wazalendo wa kuipenda…
Watumishi wanaofanya kazi katika idara mbali mbali za serikali wametakiwa kuacha tabia ya kuiponda serikali na badala yake wawe wazalendo wa kuipenda nchi yao kwa kuzungumzia maendeleo ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Daktari JOHN MAGUFULI.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI,GEORGE KAKUNDA wakati wa ziara yake wilayani IGUNGA ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema watumishi wana wajibu wa kuzungumzia mafanikio yanayofikiwa na serikali ukiwemo ujenzi wa reli kutoka ya kisasa kutoka DAR ES SALAAM kwenda mikoa ya MOROGORO,DODOMA,TABORA hadi MWANZA,ujenzi wa bomba la mafuta kutoka HOIMA-UGANDA hadi TANGA na usimamiaji wa ujenzi wa viwanja vya ndege na bandari.
Naibu Waziri KAKUNDA ametembelea baadhi ya miradi ya serikali iliyopo katika shule ya sekondari NANGA ukiwemo ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila moja, madarasa manne na matundu kumi ya vyoo,vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 241.
Pia ametembelea shule ya sekondari ZIBA ambapo kuna miradi ya ujenzi wa bweni la wavulana,ujenzi wa mabweni mawili,madarasa mawili na kutembelea mradi wa bomba la maji lililopo katika kata ya MWISI wilayani IGUNGA.
Baada ya kutembelea miradi hiyo,KAKUNDA amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya IGUNGA,REVOCATUS KUULI kuwaandikia barua ya pongezi walimu wakuu wa shule hizo kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.