
TANZIA: Radio wa Kundi la Goodlife afariki dunia
Msanii wa muziki kutoka nchini Uganda, Radio amefariki dunia. Msanii huyo ambaye alikuwa akifanya vizuri na mwenzie
Weasel, tangu January 23 mwaka huu hali yake ilikuwa ikiripotiwa kuwa mbaya kufuatia majereha aliyoyapata kutokana na ugomvi wa klabu.
Hapo jana Rais wa Uganda, Yoweri Museven alitoa Milioni 30 kwa ajili ya matibabu ya msanii huyo, pia kulikuwa na maombi maalumu yalikuwa yameandaliwa kwa ajili ya kumuombea ambayo yalitarajiwa kufanyika February 4 mwaka huu katika kanisa la Light the World.
Bw Balaam Barugahara, ambaye ni promota, anasema kuwa Radio alifariki dunia Alhamisi majira ya saa kumi na mbili asubuhi.
Radio alifariki katika hospitali ya Case mjini Kampala ambako alikuwa amelazwa baada ya kuripotiwa kupigwa hadi kupoteza fahamu kwenye kilabu cha pombe cha De Bar, kilichopo katika mji wa Entebbe wiki iliyopita.
“Utawala wa hospitali ya Case wanasikitika kutangaza kifo cha Moses Ssekibogo alias Moze Radio leo tarehe 1 Februari 2018 saa kumi na mbili asubuhi,” ilisoma sehemu ya taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Case kuhusiana na kifo hicho.
“Nimeelezwa juu ya kifo cha mwanamuziki Moses Ssekibogo aka Mowzey Radio. Hivi karibuni nilitoa mchango wangu kwa ajili ya matibabu yake nikitumaini kwamba atapona. Alikuwa kijana mdogo mwenye kipaji mwenye maisha mazuri ya mbeleni,” Alielezea Museveni katika ujumbe wa Twitter.
Hii inakuja saa chache baada ya rais Museveni kuchangia Shilingi milioni 30m, pesa za Uganda kwa ajili ya matibabu yake.
”Wakati Mowzey Radio alipoingia kwenye uwanja wa Muziki, sekta ya muziki ilikua mahututi. Muziki wa wanamuziki wachache wa waliokuwa maarufu zaidi wakati huo ulikua umerudiwa rudiwa kupita kiasi na kuchosha .Ninyi wawili mlikuja kwenye sekta hii na kuiongezea uhai sekta ya muziki. Mlileta ushindanikwa miziki mizuri na uvaaji mpya ,” Alituma ujumbe Liz Elder kwenye ukurasa wa Facebook.
Vipaji vya Radio vya Uimbaji pamoja na muziki vilianza kubainika wakati alipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari, akiimba katika kwaya ya kanisa katoliki. Akiwa mwanafunzi wa sekondari pia aliweza kujizolea tunu mbali mbali za uimbaji katika ngazi ya wilaya na nyingine nyingi.
Radio alipendwa sana kwa utumbuizaji wake kwenye sherehe na tamasha mbali mbali za muziki na za kijamii kwa sauti yake thabiti na ya kuvutia.
Wiki iliyopita, polisi walisema kuwa waliwakamata watu watano kwa ajili ya kuisaidia katika uchunguzi wa polisi juu ya kisa cha kumpiga Radio.