Ukatili wa kingono mkoani TABORA bado ni tatizo kutokana…
Ukatili wa kingono mkoani TABORA bado ni tatizo kwa sababu wahanga wa matukio hayo huyaficha na kuyamaliza katika ngazi ya familia bila kuyapeleka sehemu husika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu- PARALEGAL mkoani TABORA,MARTHA SIZYA kesi nyingi za ukatili wa kingono haziripotiwi kwenye vyombo vya sheria kwa sababu waathirika wanaona aibu kwa kutojua haki zao za msingi.
MARTHA SIZYA pia amezungumzia wajane wanaodhulumiwa mali na kufukuzwa kwenye nyumba zao na kuwataka wajane wasikae kimya kwani huo ni ukatili unaotakiwa kupigwa vita na kila mwananchi.
Naye mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya TABORA,JENI KAZAI amekiri kuwa vitendo vya ukatili wa kingono hasa kwa watoto vimeshamiri kwa sababu baadhi ya wazazi huwaacha watoto wao katika mazingira yasiyo salama na kwenda kwenye shughuli zao za kibiashara.
Ukatili wa kingono ni tishio la haki ya kila mtu ya kuishi kwa amani na usalama, hivyo kuna kila sababu ya kudhibiti tatizo hilo katika jamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch,hapa TANZANIA,kati ya watoto watatu kike,mtoto mmoja hufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono.