
Vijana wametakiwa kutoogopa kwenda katika vituo na zahanati ambazo…
Vijana wametakiwa kutoogopa kwenda katika vituo na zahanati ambazo zinatoa huduma rafiki kwao ili kupata huduma za ushauri nasaha zitakazowasaidia kuepukana na mimba za utotoni.
Hayo yamebainishwa na Muuguzi msaidizi wa zahanati ya CHEYO,BERTHA KULWA wakati akizungumzia mwitikio wa vijana kwenda katika vituo vinavyotoa ushauri nasaha na huduma ya afya ya uzazi kwa vijana akisema mwitikio wao bado ni mdogo.
Naye Muuguzi wa zahanati hiyo,GRACE SHIMBA amezitaja sababu zinazosababisha vijana kuanza ngono katika umri mdogo ambazo iwapo vijana wakipata ushauri nasaha ni rahisi kutambua jinsi gani wanaweza kuepukana na sababu hizo.
Kwa upande wao,viongozi wa madhehebu ya dini,Mchungaji wa kanisa la CVC -VICTORIUS lililopo mtaa wa KADINYA,EGON ISRAEL na Sheikh wa wilaya ya TABORA,RAMADHAN RASHDI wamesema wanaendelea kuwahamasisha vijana na walezi kuzingatia maadili na maagizo ya Mwenyezi Mungu na kufanyia kazi ushauri wanaopewa.
Mwaka 2016 mkoa wa TABORA ulianza kutoa huduma rafiki kwa vijana,afya ya uzazi kwa vijana,taarifa sahihi ya unasihi ya afya ya uzazi,kutambua mabadiliko yao ya kimwili,upimaji wa afya ,uchunguzi wa magonjwa ya ngono,saratani ya mlango wa uzazi na matiti,matibabu ya magonjwa ya ngono na huduma bora ya ujauzito.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya TABORA vituo vinavyotoa huduma hizo ni CHEYO,TOWN KLINIK,KITETE na ISEVYA.
Mwandishi:- Eveline Paul.