Wananchi wa Kata ya Loya Wilaya ya Uyui Mkoani…

Wananchi wa kata ya LOYA,wilaya ya UYUI mkoani TABORA wameliomba Jeshi la Polisi kupunguza masharti na vigezo ili waweze kufungua kituo cha polisi katika kata yao.
Akitoa ombi hilo kwa Kamanda wa polisi mkoa wa TABORA, Afisa Mtendaji wa kata ya LOYA, NDULILAH PANDAUYAGA amesema iwapo kituo cha polisi kitafunguliwa katika kata hiyo kitasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.
Diwani wa kata ya LOYA,SIZYA MASELE amesema kufunguliwa kwa kituo cha polisi katika kata yake kutasaidia kuimarisha hali ya ulinzi na usalama na kujenga woga kwa wahalifu kutoka ndani na nje ya kata hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya UYUI, SAID NTAHONDI amesema halmashauri imeunga mkono jitihada za wananchi wa LOYA na tayari imekwishatoa edha kwa ajili ya kumalizia jengo la kituo cha polisi.
Akikagua jengo la kituo hicho,Kamanda wa polisi mkoa wa TABORA Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi,WILBROAD MUTAFUNGWA amesema jengo hilo lina mapungufu kidogo na iwapo yatarekebishwa basi baada ya wiki moja litafunguliwa rasmi kama kituo cha polisi.
Wananchi wa vijiji vya LOYA,MISWAKI,MMALE,MINYEZE na LUTENDE wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 100 kufuata huduma za kipolisi.